Ijumaa 3 Julai 2026 - 01:00
Hizbullah Yawapinga Wanaounga Mkono Uhuru wa Lebanon Kupitia Makubaliano ya Maridhiano na Israel

Hawza/ Baada ya kupita siku kadhaa tangu kutangazwa kwa makubaliano ya maridhiano kati ya serikali ya Lebanon na Israel, makundi mbalimbali ya kijamii na vyama vya kisiasa vya Lebanon yameeleza kuwa makubaliano hayo ni maandalizi ya kuanzisha vita vya wenyewe kwa wenyewe na kuuwezesha utawala wa Kizayuni kuikalia ardhi ya Lebanon.

Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, katika hali ambayo wananchi wa Lebanon, hususan walioko kusini mwa nchi hiyo, kila siku wanakabiliwa na mashambulizi ya utawala wa Kizayuni na wanahangaika na maisha ya ukimbizi, serikali ya Lebanon, bila kujali maandamano makubwa ya kupinga hatua hiyo, ilitia saini makubaliano ya maridhiano na utawala wa Kizayuni. Makubaliano hayo hayakukataliwa tu na Mashia na wafuasi wa Hizbullah, bali pia makundi mbalimbali ya kisiasa yalitoa tathmini mbaya sana dhidi yake.

Hanna Gharib, Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomunisti cha Lebanon, alikosoa vikali mchakato wowote wa kuhalalisha uhusiano na utawala wa Kizayuni, akisisitiza kwamba; wananchi wa Lebanon watayakataa makubaliano yoyote yatakayodhoofisha mamlaka ya kitaifa na kuimarisha ukaliaji wa ardhi yao.

Chama cha Kisoshalisti cha Kitaifa cha Lebanon kilisema katika taarifa yake kwamba; wakati ambapo mashujaa wa muqawama wanaandika historia ya kishujaa iliyojaa ujasiri, ushujaa na kujitolea, na wananchi wa Lebanon wanatoa maisha yao kwa ajili ya kulinda heshima na mamlaka ya nchi yao huku wakiteseka kutokana na uharibifu na ukimbizi, na wakilipa gharama hiyo kwa damu zao, ukimbizi na maangamizi, maafisa rasmi wa Marekani wamekubali kushiriki katika tukio la fedheha linaloitwa "Mkataba wa Mfumo wa Pande Tatu", ambao unasimamiwa na kuamuliwa na serikali ya Marekani, serikali ambayo yenyewe ni mshirika katika uvamizi na vita dhidi ya wananchi wa Lebanon.

Kwa mujibu wa ripoti ya Al-Ahed, Ihab Hamadeh, mbunge na mwanachama wa Kambi ya Uaminifu kwa Muqawama, anaamini kwamba msimamo wa Nabih Berri, Spika wa Bunge la Lebanon, ulikuwa wa wazi na thabiti alipoligeuza suala hili kuwa mfano halisi wa kile kilichoitwa mfumo wa maelewano wa pande tatu kati ya serikali, adui na Wamarekani. Alisema kuwa lengo pekee la "mfumo" huo ni kuwafanya Walebanon wapigane wao kwa wao kwa manufaa ya Waisraeli, na baada ya hapo kuwe na sehemu ambayo utawala huo unaweza kupumzika ndani yake, nayo ni kusini mwa Lebanon. Akaongeza kuwa; hakuna anayejua ni nani atakayehusika katika mapambano hayo, na kwamba Lebanon ipo katika hatari kubwa.

Alisisitiza kwamba; kamari ambayo serikali hii imeingia si kamari dhidi ya muqawama au silaha zake, bali ni kamari dhidi ya Lebanon yenyewe, akaongeza kuwa; Walebanon wote wanapaswa kufahamu kwamba serikali hii imeweka matumaini yake katika migawanyiko ya ndani kwa ajili ya hatua ya mwisho ya mchezo huu. Alisema: "Kile kilichoitwa 'Mfumo wa Makubaliano' tayari kimesambaratika, na hati hii ilizaliwa ikiwa tayari imeungua na kufa, kwa sababu serikali hii haiwezi kuiingiza nchi katika vita vya wenyewe kwa wenyewe, wala haiwezi kuwapatia Waisraeli kile ambacho hawakuweza kukipata vitani. Aidha, haina uhalali wa kukabidhi hata chembe moja ya mchanga, sembuse ardhi ya Lebanon."

Najah Wakim, mwanzilishi wa Harakati ya Umma, alisema kwamba; kila anayeyaunga mkono makubaliano yaliyotiwa saini mjini Washington kati ya viongozi wa Lebanon na adui Muisraeli anatambua jinsi yalivyo hatari na mabaya. Aliongeza: "Wale walioandaa makubaliano haya nje ya nchi (Marekani na Israel) na wale waliotia saini ndani ya Lebanon wanajua kwamba hayatapitishwa. Basi kwa nini yalitiwa saini? Lengo lake ni kuiingiza nchi katika mzozo."

Wakim, baada ya kukutana na Rais wa Bunge Nabih Berri huko Ain al-Tineh, alisema: "Sasa swali si tena kama uko upande huu au ule, au kama unaunga mkono silaha au hauungi mkono. Maswali hayo yote hayana nafasi tena. Sasa kuna swali moja kuu linalowaelekea Walebanon wote: Je, mnakubali vita vya wenyewe kwa wenyewe au mnavikataa? Kwa hiyo, suala hili linahitaji kazi kubwa, busara nyingi, ujasiri mkubwa na juhudi zilizoratibiwa ili kuzuia nchi isivutwe katika mzozo ambao Wamarekani na Waisraeli wanaukusudia."

Akijibu swali kuhusu iwapo makubaliano ya sasa ni hatari zaidi kuliko Makubaliano ya tarehe 17 Mei, Wakim alisema: "Makubaliano haya ni hatari zaidi kwa kuzingatia mazingira ya sasa, wakati ule lengo lilikuwa kuisukuma Lebanon kuelekea 'amani' na Israel, lakini leo lengo ni hatari zaidi kuliko hilo, kusudio ni kuigawa Lebanon kupitia vita vya wenyewe kwa wenyewe, kwa hiyo mazingira ya sasa ni ya hatari zaidi, vifungu vya wazi vya makubaliano haya, hata kabla ya kufikia vifungu vya siri ambavyo navyo vinaeleweka wazi, vinaelekeza jukumu hilo kwa jeshi, wanafahamu kwamba jeshi likibebeshwa mzigo huo, basi hatari itageuka kuwa tishio kwa umoja wa jeshi lenyewe, hivyo mgawanyiko kama huo utaishia kwenye nini?"

Kwa upande mwingine, wananchi wa Lebanon, licha ya kuishi katika mazingira magumu ya ukimbizi, pia wanayapinga makubaliano haya ya maridhiano, wanasema wanapendelea kuishi kwa heshima katika mazingira ya vita na ukimbizi kuliko kuishi chini ya hali ya nchi yao kukaliwa na majeshi ya kigeni.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha